
Afrika yaaswa kuungana kuimarisha elimu mtandao, mifumo na uchumi wa kidigitali
Na Fred Kibano, D'Salaam
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amefungua kongamano la Kimataifa la elimu mtandao Afrika na kuzitaka nchi za Afrika kuungana ili kuleta mapinduzi ya elimu mtandao na kujenga uchumi wa kidigitali.
Mheshimiwa Dkt. Biteko ameyasema hayo leo wakati akifungua kongamano la Kimataifa la 18 la elimu mtandao kwa Afrika ‘eLearning Africa’ kwa niaba ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam leo tarehe 7 Mei, 2025 Jijini Dar es Salaam na kutoa wito kwa nchi za Afrika kuungana pamoja ili kuleta mapinduzi ya elimu mtandao na kujenga Uchumi imara wa kidigitali miongoni mwao.
“mustakabali wa Afrika ni kuungana pamoja na kuimarisha miundo ya ushirikiano inayoruhusu uundaji wa suluhu za kidigitali zinazolengwa kulingana na mahitaji ya Afrika ambayo yatasaidia kuleta mageuzi ya kidijitali ambayo ni jumuishi na yenye matokeo, kushughulikia changamoto mahususi zinazokabili kanda mbalimbali na kuchangia ustawi wa muda mrefu wa Afrika” alisema Biteko.
Aidha, ameitaka Afrika kuendelea kuelimisha na kuendeleza rasilimali watu, kuwashirikisha wataalamu wenye ujuzi ndani na nje ya Afrika ili kuchangia kujenga uchumi imara wa kidigitali ambao utasaidia kuongeza uwezo wa kujitegemea na kuwezesha ukuaji endelevu wa uchumi wa kidijitali.
Kwa upande wake Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema lengo kuu la elimu mtandao kwa Afrika (ELearning Africa) ni kupanua ufikaji wa elimu na mafunzo bora lakini pamoja na maboresho ya Sera ya Elimu, Serikali imewekeza katika uwezo wa kimsingi kupitia ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi, inawezesha pia walimu, Viongozi wa shule na wakufunzi kujumuisha teknolojia katika ujifunzaji, huku ikichunguza matumizi ya AI katika ujifunzaji ambayo pia itasaidia katika utungaji Sera.
“Hatua muhimu ni Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya 2014 iliyosasishwa (toleo la 2023), ambayo inatanguliza ujumuishaji wa kidijitali katika ufundishaji na ujifunzaji. Hii inakamilishwa na Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Dijiti na Miongozo ya utekelezaji, ikijumuisha ile ya matumizi ya AI katika elimu” anasisitiza Prof. Mkenda.
Kongamano hilo linalofanyika kwa mara ya pili hapa nchini limewakutanisha wadau zaidi ya 1500 wa Sekta mbalimbali kutoka nchi za Afrika pamoja na Wadau wa Maendeleo wakiwemo wataalamu, wabunifu, watafiti, wawekezaji na wafanyabiashara ili kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kupanga mikakati ya pamoja kama Afrika jinsi ya kutumia teknolojia ya kidigitali katika kuendeleza Sekta ya Elimu kwa ajili ya kujiletea maendeleo likiwa na Kauli Mbiu inayosema “Kufikiri Upya Elimu na Maendeleo ya Rasilimali Watu kwa ustawi wa Baadae wa Afrika”
Comments
Please sign in to leave a comment.