
Majaliwa: toa iwe sehemu ya mabadiliko chanya kwenye serikali za mitaa
OR - TAMISEMI
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ameeleza uimarishaji wa Taasisi ya Maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa(TOA) ili iwe na nguvu na iweze kuishauri Serikali ipasavyo.
Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Aprili 14, 2025 wakati akifungua mkutano wa 15 wa TOA unafanyika katika Ukumbi wa Jiji mkoani Dodoma.
Amesema viongozi wa Kitaifa wanaitaka taasisi hiyo kuwa sehemu ya mabadiliko chanya ya mwelekeo wa utendaji ili ichagize maboresho katika Serikali za Mitaa.
”Endeleeni kuhimiza wanachama kufanya kazi kwa weledi na uzalendo ili kuleta matokeo yanayotarajiwa na wananchi.”
“Kwa kuzingatia ukaribu na ushirikiano wenu na wananchi, naamini mnazitambua changamoto zinazowakabili na mnaelewa afua ambazo zikitekelezwa zitawaletea maendeleo. "
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema Serikali imesimamia matumizi ya mifumo ya kieletroniki ili kuimarisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mifumo hiyo ni pamoja na Mifumo ya Uhasibu, Mifumo ya ukusanyaji wa mapato, Manunuzi na Malipo.
"Matumizi ya Mifumo yamesaidia kupunguza urasimu, kurahisisha ulipaji wa malipo na kodi mbalimbali za Serikali na kuboresha ukusanyaji wa mapato hadi kufikia ukusanyaji wa zaidi ya shilingi bilioni 900."
Pia ametumia fursa hiyo kuagiza uongozi wa TOA uwajibike kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutanua wigo wa mapato ili kuongeza uwezo wa kujitegemea kimapato na kugharamia shughuli mbalimbali za uendeshaji na utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amewataka viongozi wote wa Mikoa na watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini, waendelee kusimamia maadili na uzalendo, mifumo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na mifumo mingine yote iliyoanzishwa na Serikali kwenye ngazi zao.
Pia amewahimiza kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za umma pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umekuwa na ufanisi zaidi katika Serikali za Mitaa.
Awali, Mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania, Albert Msovela alisema wataendelea kusimamia taasisi hiyo na kuhakikisha wanatekeleza shughuli zote za Serikali kwa weledi na ufanisi mkubwa.
Comments
Please sign in to leave a comment.