
Mchengerwa: Rufiji ina ndoto ya kuwa na majengo ya ghorofa hospitali ya Utete
Na OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema wananchi wa Rufiji wana ndoto ya kuwa na majengo ya ghorofa yatakayoinua viwango vya utoaji huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Utete.
Kauli hiyo ameitoa akiwa katika Hospitali hiyo kabla ya kumkaribisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Taifa, Ismail Ussi, kuzungumza na wananchi mara baada ya Mwenge wa Uhuru kukagua ukarabati uliofanyika katika hospitali hiyo muhimu kwa wakazi wa Rufiji.
“Kutokana na kasi ya maendeleo inayosukumwa na Mheshimiwa Rais kwa wananchi wa Rufiji, tuna ndoto ya kupata majengo ya ghorofa katika hospitali yetu ya wilaya, na tunayo ardhi ya kutosha kwa ajili ya ujenzi huo,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Aidha, amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutolewa sh. milioni 850 kwa ajili ya kuongeza majengo katika Hospitali hiyo ya Wilaya, hatua itakayoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na fedha hizo zinatarajiwa kupokelewa ndani ya mwezi huu wa Aprili.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa wananchi wa Rufiji wana matarajio makubwa ya maendeleo, na kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaamini maendeleo hayo yataendelea kushamiri katika maeneo yote ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Taifa, Ismail Ussi, amesema kuwa maendeleo yaliyofanywa Rufiji, hususan ukarabati wa Hospitali ya Wilaya Utete, ni kielelezo tosha cha mafanikio ya Mwenge wa Uhuru ambao unahimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
“Sisi wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa tumeridhishwa na ukarabati na maboresho yaliyofanyika hapa Hospitali ya Wilaya ya Utete, na tunasisitiza huduma ziendelee kutolewa kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa jitihada hizi,” amesema Ussi.
Comments
Please sign in to leave a comment.