
TRIL.1.29/- ZIMEWEKEZWA NGAZI YA AFYA YA MSINGI– Mhe. Dkt. Dugange
Na OR - TAMISEMI, Dodoma
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imewekeza Sh.Trilioni 1.29 kwenye ngazi ya afya ya msingi pekee.
Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Nchi-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwenye kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Afya ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwaka huu kwa lengo la kutambua mchango wa sekta ya afya, kuimarisha uelewa wa jamii, na kutathmini maendeleo yaliyopatikana, yakiwa na kauli mbiu “Tulipotoka, Tulipo, Tunapoelekea; Tunajenga Taifa Imara na lenye Afya.”
Dkt. Dugange ameeleza kuwa fedha hizo zimetumika kuboresha miundombinu na vifaa tiba katika vituo vya afya, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mashine za mionzi za kawaida na za kidigitali (Digital X-ray), pamoja na vifaa vya upasuaji vilivyoongezwa katika vituo 21 vya afya nchini.
Vilevile, amesema Serikali imeimarisha mawasiliano na mshikamano kati ya ngazi ya afya ya msingi na rufaa ili kuondoa usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakihitaji huduma za kibingwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Dugange ameeleza kuwa katika kipindi hicho hospitali 129 za Halmashauri zimejengwa, pamoja na vituo vya afya 367, majengo ya huduma za dharura 87, ICU 30, mitambo ya hewa tiba (oxygen plant) 21, na nyumba za watumishi 270. Aidha, hospitali kongwe 50 zimekarabatiwa, maboma ya zahanati 980 yamekamilishwa, na magari 560 yamenunuliwa, yakiwemo magari ya wagonjwa 382 na magari ya usimamizi shirikishi 212.
Ameongeza kuwa jitihada hizo zimechangia kupungua kwa vifo vya akinamama wakati wa kujifungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 miaka mitano iliyopita hadi kufikia 104 mwaka 2024 na kwamba hilo ni zao la uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ya msingi nchini.
Comments
Please sign in to leave a comment.
Tangazo la kuitwa kazini ajira za TMCHIP 2025
Mpango Mkakati wa Usimamizi wa Takwimu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI - 2024/25 -2028/29
Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji 2024
Kanuni za Uchaguzi wa mwaka 2024
Tangazo la Uchaguzi




