
Uandikishaji wa wanafunzi ufanyike bila kujali tofauti zao’ mhe mchengerwa
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaagiza Viongozi wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha uandikishaji wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari unafanyika bila kujali tofauti zao za kiafya na kimaumbile.
Mhe. Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo Januari 6, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi vyumba 18 vya madarasa vilivyogharimu Shilingi milioni 300 katika Halmashauri ya Wiaya ya Bahi ambapo pia ametoa tuzo kwa waandishi 15 wa habari za Mradi wa Shule Bora.
'Nawaagiza mkasimamie kwa dhati zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wote bila kujali tofauti zao za kiafya na kimaumbile wenye umri lengwa kwa ajili ya kuanza darasa la awali, msingi na MEMKWA' amesisitiza.
Mchengerwa amewataka Viongozi hao kutoa takwimu sahihi za uandikishaji na jinsi wanavyoripoti wanafunzi katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Kila siku ya Ijumaa katika wiki).
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Elimu ambayo yameleta matokeo makubwa ikiwemo kuongeza ufaulu Dodoma kwa shule za msingi na sekondari na kupunguza utoro kutoka wanafunzi 24,000 hadi 6,000 (2024).
Akitoa taarifa kuhusu umalizaji wa ujenzi wa madarasa hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bahi, Zaina Mlawa alisema ujenzi wa madarasa 10 umefanyika kwa kufuata mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ambao unalengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Naye Mwakilishi wa Balozi kutoka ubalozi wa Uingereza, Sally Hedley alisema elimu ni kipaumbele kwa serikali hiyo hivyo nchi hiyo itaendelea kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuweka miradi rafiki ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa wanafunzi.
Mradi wa Shule Bora umejikita katika kuboresha elimu ya awali na msingi kwa katika maeneo manne ya ujifunzaji, ufundishaji, ujumuishi na uimarishaji wa mifumo na ulizinduliwa rasmi na Vicky Ford (Parliamentary Under Secretary State-UK) Aprili 4, 2022 katika shule za Msingi Mkoani iliyopo Kibaha- Pwani. Mikoa unapotekelezwa Mradi ni Dodoma, Singida, Pwani, Tanga, Simiyu, Kigoma, Katavi na Rukwa ambapo uchaguzi wa mikoa hii ulizingatia mambo mbalimbali ikiwemo ufaulu usioridhisha wa wanafunzi katika mitihani ya kuhitimu darasa la saba na ile ya upimaji wa darasa la Nne, utoro na mimba za utotoni.
Comments
Please sign in to leave a comment.
Tangazo la kuitwa kazini ajira za TMCHIP 2025
Mpango Mkakati wa Usimamizi wa Takwimu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI - 2024/25 -2028/29
Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji 2024
Kanuni za Uchaguzi wa mwaka 2024
Tangazo la Uchaguzi




